MAELFU ya Wana CCM wakiwa katika msafara wa mapokezi ya Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Hassan Mwinyi kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar. |
MAELFU ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na
Wananchi kwa ujumla kisiwani wamejitokeza kumpokea Mgombea Urais wa Zanzibar kwa
tiketi ya CCM Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi,aliyewasili nchini kwa mara ya
kwanza toka achaguliwe kushika nafasi hiyo.
Dkt.Hussein amewasili katika Kisiwa cha
Unguja leo majira ya saa 3:43 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid
Amani Karume na kupokelewa na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.
Baada ya kupokelewa makundi mbali mbali ya
wanachama yakiwemo ya sanaa pamoja na vijana wa CCM wakiongozwa na kikundi cha pikipiki
maalum waliongoza msafara wa kuelekea katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwanduzi
Zanzibar, ambapo hafla ya mapokezi ndipo ilipofanyika.
Alipofika katika viunga vya Ofisi hiyo alipokelewa
na vijana maalum wa chipukizi na kumvisha sikafu kwa ajili ya kumkaribisha na
baada ya hapo alikabidhiwa vifaa mbali mbali na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi na
akazuru kaburi la Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza katika hafla hiyo amesema baadhi
ya watu wanadai kuwa Dkt.Hussein sio mzawa wa Zanzibar wanapotosha kwani
kiongozi huyo kwa mujibu wa sheria za nchi ni mzaliwa wa Zanzibar na wazazi
wake wote wapo.
"Kuna watu tayari wameanza siasa chafu
za kuchafuana eti Dkt.Hussein sio mzawa je wao wamezaliwa wapi, wakati sote
tunamjua kiongozi huyu kuwa hapa ndio kwao",. amehoji Dk.Shein.
Amesema sifa alizonazo Dkt.Hussein ni nyingi
sana zikiwemo upole,uadilifu,utiifu na kuheshimu kila mtu kwa nafasi yake mambo
ambayo ni sifa za msingi za kiongozi bora.
Amesema kuchaguliwa kwa Dkt.Hussein
kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ndio maendeleo ya
CCM ya sasa na yajayo yatakayoendelea kuipaisha nchi kiuchumi.
Pamoja na hayo ameeleza wazi kuwa Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu utafanyika kwa fedha za ndani za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ),mara Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC) itakapotangaza muda rasmi wa
kuanza mchakato wa uchaguzi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi, akizungumza katika mapokezi hayo
alisema CCM itaendelea kuwa kinara wa Demokrasia.
Naye Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya
CCM Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa endapo atapata
ridhaa ya kuwa Rais wa Zanzibar ataendelea kulinda Amani na Utulivu wa Zanzibar
kwani ndio msingi wa maendeleo yote.
Amesema atalinda na kuenzi tunu za taifa
zikiwemo Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Amesema uchaguzi ndani ya CCM tayari umeisha
na makundi yote yameisha na kwa sasa limebaki kundi moja la kuiletea ushindi
CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
" Nitahakikisha suala la
upemba,uunguja,ukaskazini na ukusini havipewi nafasi kwani vinaweza kukwambisha
kasi ya maendeleo yetu", amesema Dk.Hussein.
Amesema nia ya kuwania Urais huo ni
kuwatumikia Wananchi wote bila ya ubaguzi kwa kuhakikisha ya wananchi yakuwa
bora.
Ameahidi kuwa katika safari ya maendeleo hayo
hatovumilia vitendo vya rushwa,ufisadi,wahujumu wa mali za umma na viongozi
watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao.
Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya
makada wa CCM walioshiriki katika kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa Urais wa Zanzibar kupitia
CCM,walisema kuwa mchakato wa kumpata mgombea huyo umefanyika kwa ufanisi
mkubwa na watamuunga mkono.
Akizungumza Shamsi Vuai Nahodha, ambaye ni
miongoni mwa makada walioshiriki mchakato wa kuomba ridhaa ya Urais kupitia
Chama alisema atamuunga mkono mgombea huyo hadi ashinde na kuwa Rais wa
Zanzibar.
Kwa upande wake Dkt.Khalid Salum Mohamed,
ambaye ni miongoni mwa makada walioshiriki mchakato wa kuomba ridhaa ya Urais
kupitia Chama, amesema ushindi alioupata Dk.Hussein ni ushindi wa Wana CCM wote
hivyo kazi iliyobaki ni kuhakikisha anashinda.
Naye Prof.Makame Mnyaa mbawara, amewaomba
wananchi visiwani humo kutambua kuwa wamepata bahati ya kuwa na mgombea mwenye
sifa za kuwa kiongozi bora.
Katika mchakato wa uchaguzi ndani ya Chama,
Dk. Hussein, ambaye ni mtoto wa rais wa awamu ya pili Al-Hajji Ali Hassan
Mwinyi, aliwashinda wagombea wengine waliofika katika mchujo wa mwisho, ambao
ni waziri kiongozi wa zamani Shamsi Vuai Nahodha na Khalid Salum Mohamed.
Katika mchakato wa ndani wa uchaguzi,
Dk.Hussein alipata jumla ya kura 129, ambazo ni sawa na asilimia 78.65, dhidi
ya kura 16 za Nahodha na 19 za Khalid Mohamed.
Awali, kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya
CCM Taifa Zanzibar, ilipendekeza majina
matano na kuyawasilisha kwa kamati Kuu. Pamoja na watatu waliofika duru ya
mwisho, wengine walikuwa Makame Mbarawa na Khamis Mussa Omar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni