Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Tanzania, Abdallah Bulembo amewataka wawakilishi, wabunge na madiwani wa majimbo ya Kusini Unguja kuthamini kazi zinazotekelezwa na mabalozi wa nyumba kumi kwani wao ndio viongozi wanaolinda maslahi ya chama hicho kwa ngazi za chini.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa Mkoa huo katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha uhai wa CCM Zanzibar, alisema mabalozi wa nyumba kumi wanafanya kazi kubwa ya kutafuta wanachama hai ambao ndio mtaji wa kisiasa wa kufanikisha ushindi wa chama hicho kwa kila uchaguzi.
Alieleza kuwa viongozi hao wa nyumba kumi ndio wanaowajua vizuri wanachama wenye uwezo na nia za kweli za kukisaidia chama hicho katika masuala mbali mbali za kisiasa hivyo wanatakiwa kuungwa mkono wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumzia mabadiliko ya chama Bulembo alisema mabadiliko hayo hayakufanyika kwa kumkomoa mtu bali yametokana na dhamira ya kukiimarisha chama kwa lengo la kuwapelekea wananchi wa mijini na vijijini maendeleo endelevu.
Alisema kutokana na mabadiliko yaliyofanywa ndani ya chama na kuweka utaratibu wa kugombea nafasi moja mtu mmoja ni moja ya mkakati wa kuhakikisha kila kiongozi anayepewa dhamana anatumikia nafasi yake kwa ufanisi .
“Wito wangu kwenu viongozi, watendaji na wanachama sote tushirikiane kufanya kazi za chama na jumuiya zetu kwa lengo la kutekeleza kwa vitendo dhana ya kuimarisha uchumi ndani ya chama na kwa mwananchi mmoja mmojo”, alisema Bulembo.
Aidha alifafanua kuwa malengo ya CCM kupitia uchaguzi wa ndani ya chama unaoendelea hivi sasa ni kupata viongozi waadilifu watakaokuwa na uwezo wa kukemea vitendo vya rushwa na makundi yasiofaa ndani ya chama bila ya woga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni