Jumatatu, 21 Novemba 2016
AWASIHI VIONGOZI WA CHAMA KUENDELEZA UTAMADUNI
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Nd. Vuai Ali Vuai amewasihi Viongozi wa ngazi mbali mbali za Chama kuendeleza utamaduni wa kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo Watendaji wao ili wawe na uelewa na ujuzi wa kutekeleza shughuli za Chama kwa ufanisi.
Akizungumza katika Ufunguzi wa Mafunzo elekezi ya Watendaji wa Chama na Makatibu wa Siasa na Uenezi kuanzia ngazi za Matawi, Wadi hadi Jimbo Wilaya ya Amani Kichama yaliyofanyika katika Hoteli ya Villa iliyopo Maruhubi Nje Kidogo ya Mjini wa Zanzibar.
Alisema mafunzo ni nyenzo muhimu inayosaidia kuwaongezea maarifa na mbinu mbadala za kiutendaji watumishi na watendaji wa taasisi ili wafanye kazi zao kwa kujiamini zaidi.
Vuai Alifafanua kuwa CCM inakabiliwa na majukumu ya Uchaguzi wa Chama na Uchaguzi Mkuu wa Dola hivyo watendaji wa chama hicho wanatakiwa wanatakiwa kuandaliwa vizuri kupitia mafunzo ya chama kwa lengo la kukumbushwa baadhi ya majukumu yao ya msingi yakiwemo matumizi sahihi ya kanuni, katiba na miongozi ya Chama kwa makada wengine.
“Tuendelee kufanya mafunzo kwa wingi kadri hali itakavyoruhusu kwani ni jambo muhimu kwa binadamu yeyote yule anayetaka maendeleo mazuri ya kazi yake kwa lengo la kuongeza ujuzi na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zetu za kisiasa ndani na nje ya Chama chetu.”, alisema Vuai na kuongeza kuwa mafunzo yatawasaidia watendaji hao kuelewa kwa upana wanayoyafanya na kuepuka athari ya kufanya kazi kwa mazoea.
Naibu Vuai alieleza kwamba utaratibu wa mafunzo umeanza zamani ambapo Chama kilikuwa na vyuo vyake maalum vya kuwaandaa makada , watendaji na viongozi makini waliokuwa na uwezo mkubwa wa kujenga hoja na kuzisimamia katika kuimarisha maendeleo ya Chama.
Alisema kwa mujibu wa ibara ya 5 ya Katiba ya Chama hicho ni kushika Dola Tanzania bara na Zanzibar serikali za mitaa na serikali kuu, hivyo amewapongeza makada hao kwa uwezo na jitihada zao za kuahakikisha kila uchaguzi toka umeanza mfumo wa vyama vingi CCM imekuwa ikishinda.
Aidha aliwataka watendaji hao kuanzia ngazi za Matawi hadi Wilaya kutumia fursa walizokuwa nazo katika maeneo yao kwa kuanzisha miradi mbali mbali itakayowasaidia kupata kipato cha kutatua baadhi ya changamoto zinazohitaji fedha na kujitegemea wenyewe badala ya kuendelea kuwategemea Viongozi wa majimbo pekee.
Hata hivyo aliendelea kuwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kwamba Watendaji watakaopata fursa ya kugawa fomu za kugombea Uongozi ndani ya CCM waongeze bidii katika kutenda haki kwa kuhakikisha kila mwanachama mwenye sifa ya kuchagua na kuchaguliwa anapata haki hiyo kwa mujibu wa ibara ya 14 ya Katiba ya Chama hicho.
“ Najua watendaji na viongozi wa CCM ni waadilifu lakini naomba tuongeze umakini katika suala la Uchaguzi wa Chama kwa kuwapatia fomu wale wote wenye Haki ya kuchagua na kuchaguliwa msiwanyime fursa hiyo kama mtu hafai basi mwacheni akanyimwe kura na wanachama wenzake lakini nyinyi msihusike na kufanya hivyo kutapunguza malalamiko .”, alisisitiza Vuai.
Naye Katibu wa Wilaya ya Amani Kichama, Abdallah Mwingi amesema lengo la mafunzo hayo kwa lengo la kuzidi kuwajengea uwezo watendaji hao ili waweze kusimamia ipasavyo Chaguzi za Chama na Dola zijazo kwa kuwachuja wanachama wanaotaka nafasi za uongozi na kuwapata viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi na sera za CCM na serikali zilizopo madarakani.
Alisema Wilaya hiyo imekuwa ikifanya kazi ya ziada ya kuimarisha chama kwa kuongeza wanachama wapya na kuwapatia mafunzo maalum kupitia madarasa ya itikadi kwa lengo la kuwajenga kuwa waumini wa kweli watakaosimamia maslahi ya CCM bila ya hofu.
Akitoa maneno ya Shukrani Mbunge wa Jimbo la Mpendae, Salim Hassan Turky, amesema washiriki hao watazifanyia kazi nasaha hizo kwa lengo la kuhakikisha CCM inaendelea kuwa Chama bora kinachokubalika kwa wananchi.
Aliwasihi watendaji hao makundi ya kukigawa chama wakati wa Uchaguzi kwani kuna baadhi ya watendaji waliowahi kusimamia chaguzi zilizopita wamekuwa wakilalamikiwa kwa kufanya upendeleo kwa baadhi ya Wagombea wanaowataka na hatimaye wanapatikana viongozi wenye sifa za kutilia shaka.
Aliwaomba washiriki hao kuwasaidia na kuwaongoza wanachama wa Chama hicho katika kuanzisha miradi midogo midogo kuanzia ngazi za Mashina hadi Mikoa, itakayoweza kuwasaidia kujiajiri wenyewe na kukuza Uchumi wa nchi.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni