TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
ITAKUMBUKWA kuwa Desemba 27, mwaka 2015, Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa Zanzibar ilikutana, chini ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.
Kama ilivyo ada, mara tu baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kupitia Msemaji wake Mkuu kilipata nafasi ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, kwa madhumuni ya kuwajuvya kwa muhtasari maamuzi yaliyofikiwa na kikao hicho.
Aidha, Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa Chama cha CUF Ismail Jussa kwa kukariri na kuripoti mazungumzo ya ndani ya kikao chetu, chenye dhamana ya kuendesha na kusimamia masuala yote ya siasa kwa upande wa Zanzibar.
CCM kinamshangaa kiongozi huyo kwa kuacha kuyazungumzia mambo yanayohusu chama chake na badala yake kuanza kufuatilia mambo ya ndani ya CCM ni dhahiri kwamba kiongozi huyo anavyoonyesha jinsi gani alivyoishiwa na kufilisika kisiasa.
Chama Cha Mapinduzi kinachukua nafasi hii kuwaomba Viongozi na Wanachama wote wa CCM na wapenda Amani na Utulivu wa nchini kuzipuuza na kuzidharau porojo (Drip) hizo za kisiasa za wapinzani zilizokosa heshima, hekima, busara, maadili na uvumilivu wa kisiasa na badala yake waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo zitakaowapatia mapato halali na kujikwamua na umasikini.
Aidha, waelekeze nguvu zaidi katika kudumisha suala zima la amani na utulivu huku wakisubiri maelekezo kutoka Vyombo vya Kisheria hususan Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza siku ya uchaguzi wa marudio, na kujiweka tayari na hatimaye kujitokeza kwa wingi siku hiyo tayari kwa kuwaipigia kura wagombea wote wa CCM.
Kama hiyo haitoshi, Chama Cha Mapinduzi kinasikitishwa na kinalaani vikali taarifa hiyo iliyotolewa na Jussa ambayo kwa hakika inaendeleza makosa ya kutoa matokea ya uchaguzi ya Chama chake (CUF) ilhali akijua kuwa Uchauguzi huo tayari ulishafutwa na Tume halali na iliyowekwa kikatiba na hivyo kuwafanya Wazanzibari wajiulize masuala yasiyopata majibu sahihi kwamba Jussa haoni kufanya hivyo sio tu ni kwenda kinyume na sheria za nchi bali pia ni kosa la jinai.
Mwisho kabisa, Chama Cha Mapinduzi kamwe haitaingilia maamuzi ya chama chocote cha kisiasa kwani chama hichi (CCM) ni kikubwa, kilichojijengea heshima kubwa kwa wananchi wa Tanzania, Barani Afrika na Duniani na kubwa zaidi ni chama pekee kinaheshimu demokrasia.
Ahsanteni.
(Waride Bakari Jabu),
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,
Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.