CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeelezea kuridhishwa kwake na maamamuzi ya
Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kutangaza siku ya kufanyika kwa uchaguzi wa
marudio kwa nafasi ya Urais, Uwakilishi na Udiwani.
Kimesema kuwa maamuzi hayo ya kufanyika uchaguzi huo Machi 20
mwaka huu, yanaenda sambamba na matakwa ya wananchi waliokuwa wengi katika
kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa mujibu wa miongozo ya katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Itikadi na
Uenezi CCM Zanzibar, Waride Bakar Jabu alisema kwamba CCM inaungana na vyama
vingine vya kisiasa nchini vilivyobaini kasoro za uchaguzi mkuu uliopita kuwa
na kasoro kwa kuunga mkono maamuzi ya ZEC kuwa ni sahihi kwani yamefuata hatua
muhimu za Kikatiba.
Waride alisema msimamo wa CCM katika Mkwamo wa kisiasa uliopo
Zanzibar ni kurudi katika uchaguzi wa marudio ili kila chama cha kisiasa
kinachoriki katika uchaguzi uliopita kiweze kupata haki ya kungia madarakani
kwa njia za halali na zinazokubalika kisheria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo
Waride alieleza kwamba maamuzi hayo ndiyo kipimo sahihi cha kuweka uzani
wa ukomavu wa kisiasa na demokrasia katika mfumo wa vyama vingi kwani lazima
kila chama chenye haki ya kushiriki katika uchaguzi kiridhike na hatua zote
zinazofanywa mpaka kupatikana kwa mshindi atakayekuwa anaongoza kwa wingi wa
kura halali.
“ Tunachukua fursa hii kuwaomba wananchi wote wenye haki ya
kupiga kura hasa wafuasi wa CCM pamoja na wananchi wote wajitokeze kwa wingi
kwenda kupiga kura Machi 20 mwaka huu.
Tukumbuke kwamba maamuzi hayo yamefanywa na Chombo chenye
Mamlaka ya kusimamia masuala yote ya Uchaguzi nchini baada ya kujiridhisha kuwa
kuna kasoro zilizotokea katika uchaguzi uliofutwa na kuona kuna haja ya kila
mwananchi kupata haki ya kuwachagua viongozi wanaowataka kwa njia huru, wazi na
zinazokubalika kisheria”. Alifafanua Waride na kuongeza kuwa uchaguzi huo ndiyo
njia mwafaka ya kumaliza mkwamo wa kisiasa Zanzibar.
Katibu huyo aliongeza kwamba pia wanaunga mkono msimamo wa
vyama vya vyote vya kisiasa vilivyokubali kushiriki uchaguzi wa marudio pamoja
ushauri wa Msajili wa Vyama vya Sisasa nchini , Frances Mtungi kwa kuvitaka
vyama vyenye usajili kushiriki katika mchakato huo ili kudumisha Demokrasia na
malengo na malengo ya vyama kutumia uchaguzi kushika Dola.
Akizungumzia suala la CUF kususia Uchaguzi wa marudio alisema
kwamba walichofanya ni mwendelezo wa migomo na kususa kwa mipango ya maendeleo inayofanywa na mamlaka za
serikali katika kufanya mipango mbali mbali ya maendeleo kwa maslahi ya
wananchi.
Alisema kwamba upinzani wa aina hiyo hauna nia njema ya
kujenga maendeleo ya nchi bali una nia malengo ya kukwamisha na kudumaza
maendeleo ya nchi kwa maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi wa kisiasa
wanaoweka mbele tamaa ya madaraka kuliko maisha ya wananchi.
“ Kila chama kina sera zake na misimamo yake sasa wao kama
wameona kususia uchaguzi wa marudio ndiyo njia ya kumaliza mkwamo wa kisiasa
Zanzibar hiyo ni juu yao, lakini sisi
tutashiriki kikamilifu ili chama chetu kipate ridhaa ya wananchi kurudi
madarakani ya kidemokrasia.
Aidha alisema chama
hicho kinaamini kwamba Uchaguzi Mkuu uliofanyika Octoba 25 mwaka 2015 ulikuwa
na kasoro nyingi zilizosababisha uchaguzi huo kukosa sifa ya kuwa uchaguzi huru
na wa haki na hatimaye kufutwa.
Kupitia taarifa hiyo Waride wamewaomba wananchi kujitokeza
kwa wingi katika mkutano wa hadhara wa mikoa minne kichama ya Unguja katika
uzinduzi wa miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM itakayofanyika katika Afisi kuu ya CCM Kisiwandui, January 31 mwaka
huu.
Alisema Mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa
Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein.
MWISHO.
Sawa
JibuFuta