Jumanne, 14 Februari 2017

CCM yakabidhiwa Kombe la Ushindi


Na Mwandishi wetu,

ZIKIWA zimetimia siku 10 tangu kuadhimishwa kilele cha kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi(CCM), ambapo leo Timu ya Tawi la Chama hicho Kisiwandui imekabidhi rasmi Kombe la ushindi kwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakar Jabu.

Hafla hiyo imefanyika kufuatia ushindi wa Timu hiyo kwa njia ya penaliti 4-2 dhidi ya timu ya Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Zenj Fleva katika mechi ya shamrashara za kuadhimisha kuzaliwa kwa chama hicho.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakar Jabu, amesema licha ya CCM kufanya shughuli za Kisiasa bado inathamini mchango wa sekta ya michezo katika kuharakisha maendeleo ya nchi.

Alisema harakati za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 zilifanywa na vijana ambao wengi wao walikuwa ni wanamichezo mashuhuri katika vilabu vya timu za hapa nchini.

Waride alieleza kuwa ushindi waliotwaa timu ya Chama hicho ni miongoni mwa utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya CCM ibara ya 5 inayosisitiza ushindi kwa kila shughuli inayofanywa chama hicho.

“Nakupongezeni sana timu yetu kwa ushindi mliotwaa licha ya maandalizi ya mechi hiyo kuwa ya muda mfupi, lakini kwa umoja na mshikamano wenu mmeweza kukijengea heshima kubwa Chama katika sekta ya Michezo.

Nakuahidini kuwa Chama chetu kitaendelea kuunga mkono juhudi zenu ili kuhakikisha taasisi yetu inakuwa na timu ya mpira wa miguu yenye uwezo na nauomba uongozi wa timu utafute mbinu ya kuanzisha timu za michezo mingine kwa lengo la kuweka uwiano wa michezo kwa makundi yote”, .alieleza Waride.

Aidha alisema kwa niaba ya Niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai anatoa wito kwa vijana kujiunga na michezo mbali mbali nchini kwa lengo la kuendeleza heshima ya Zanzibar kimichezo.

Alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 inatambua umuhimu wa michezo katika kukuza na kuinua uchumi na maendeleo ya nchi, hivyo ni miongoni mwa sekta inayotakiwa kusimamiwa kikamilifu bila ya kuingiza mitizamo na itikadi za kisiasa.

Amezitaka taasisi zenye dhamana ya Michezo nchini kujitathimini na kufanya utafti wa kuibua vikwazo vinavyopelekea kukwamisha juhudi za maendeleo ya sekta hiyo na kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwa maslahi ya wananchi wote.

Mapema akisoma risala Afisa mwandamizi wa Masuala ya Michezo na Ufundi wa Timu hiyo, Mzee Abdallah Khatib ameupongeza uongozi wa Afisi kuu wa kuwaunga mkono toka mwanzo walipowasilisha wazo la kuundwa kwa timu itakayocheza mechi ya shamrashara ya kuzaliwa kwa CCM.

Alieleza kuwa pamoja na juhudi na umoja ulipo ndani ya timu hiyo bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya michezo zikiwemo mipira, jezi, koni, dawa za matibabu (first Aids Kit) na usafiri wa kuwafikisha katika sehemu watakazokuwa wanaenda kucheza mechi za kirafiki.

Naye Meneja wa Timu hiyo Nadra Juma Mohamed alisema lengo la kuanzisha timu hiyo ni kuendeleza umoja na ushirikiano baina ya ngazi mbali mbali za Chama na Jumuiya ili kupata sehemu mbadala ya kubadilishana mawazo.

“ Tunaomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wetu mbali mbali wakiwemo Wabunge, Wawakilishi na Madiwani waje kutuunga mkono kwani jahazi tunalosafiria ni moja katika kulinda maslahi ya chama chetu, huku tukiwa karibu na kundi la vijana kimichezo.”, alisisitiza Meneja huyo.

Hata hivyo, aliwashukru viongozi wa CCM na Taasisi mbali mbali zilizosaidia kufanikisha mechi hiyo.

Akitoa Nasaha zake Kocha wa Timu hiyo, Othman Kibwana aliuomba uongozi wa CCM Afisi kuu Zanzibar kuwakutanisha na Timu mbali mbali zikiwemo za Bunge la Jamhuri ya Muungano, Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili waweze kucheza nao mechi za kirafiki kwa lengo la kudumisha mahusiano mengi kwa taasisi hizo.

Mechi hiyo iliyochezwa Februari 3 mwaka huu baina ya Timu ya Tawi la CCM Zanzibar na  Wasanii wa Zenj Fleva ambapo timu ya Chama hicho ilitwaa Kombe, pea moja ya jezi na mpira mmoja wa miguu huku wapinzani wao wakipata pea moja ya jezi.

Hafla hiyo iliudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Chama na Jumuiya akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama Bora afya Silima Juma, Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini Fatma Juma Shomari, Katibu Msaidizi Jumuiya ya Wazazi Zanzibar Mustafa Rashid Malwa, Kaimu Afisa Utawala Mkuu wa CCM Zanzibar Mwenemzi Omar Said na Katibu wa Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Haji Mkema Haji.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni