Jumanne, 12 Desemba 2017

DKT.MAGUFULI ASIKITISHWA MPOROMOKO WA MAADILI, AZISHUKIA TCRA NA WIZARA YA HABARI

 MWENYEKITI wa CCM Taifa, Dkt. John Pombe Magufuli akifungua Mkutano wa Tisa wa Umoja wa Wazazi CCM Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa JK -Dodoma.



NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.

MWEYEKITI wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Dkt. John Pombe Magufuli ameuagiza Umoja wa Wazazi Tanzania kusimamia kikamilifu maadili na malezi ya kijamii nchini.

Agizo hilo amelitoa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja huo uliofanyia leo Mjini Dodoma, amesema viongozi watakaochaguliwa kupitia mkutano huo ambao ni maalum kwa ajili ya uchaguzi wakemee vitendo vya mmonyoko wa maadili na kurejesha mfumo wa malezi bora katika jamii.

Amesema kuwa ni aibu kuona maadili ya kijamii yaporomoka wakati CCM ina chombo chake ambacho ni Umoja wa Wazazi ambao kwa mujibu wa Katiba ya Chama umoja huo una wajibu wa kusimamia suala la maadili ya kijamii ili kujenga nchini yenye watu waojiheshimu na kuheshimiwa na mataifa mengine.

Kupitia hotuba yake hiyo Dkt. Magufuli amehoji wajibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yenye mamlaka ya kufungia chombo chochote cha habari kinachoonyesha, kutangaza na kutoa taarifa zinazokwenda kinyume na maadili ya Kitanzania na kuwataka kuchukua hatua mara moja.

Pia ameitaka Wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo kujitathimini kisha kuchukua hatua kwa kuhakikisha wanadhibiti vitendo vyote vinavyohatarisha maadili ya kijamii nchini.

“ Umoja wa wazazi simamieni maadili ya nchi yetu na hilo ni moja ya jukumu lenu, kama mnashindwa kuchukua hatua basi pigeni japo kelele na kukemea wapo watu watakusikieni na kubadilika kitabia lakini sio kukaa kimya huku nchi inaangamia.

Hivi sasa mzazi unashindwa hata kuangalia TV ukiwa na watoto wako kutokana na picha chafu za baadhi ya watu wanaokuwa wakicheza wakiwa wamevaa nusu uchi.”, amesema Dkt. Magufuli na kuhoji TCRA na Wizara ya habari kwa nini hawachukui hatua hata ya kuvifungia vyombo vya habari vinavyochangia kuporomoka kwa maadili.

Dkt. Magufuli ambaye pia ni Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amewasisitiza Wajumbe wa Mkutano Mkuu huo kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaomaliza haraka changamoto zinazokabili umoja huo.

“ Usimchague mtu kwa ajili ya mtu mwingine wala fedha zake bali chagueni viongozi imara wenye uthubutu na ujasiri wa hata kuikosoa na kuielekeza serikali mambo mema yenye manufaa kwa wananchi wote”, amesisitiza Dkt. Magufuli.

Amesema yeye ni Mwenyekiti wa Chama hicho hana kiongozi yeyote wala kundi analolipigia debe lichaguliwe hivyo  kiongozi yeyote atakayechaguliwa kwa njia ya halali ndiye atakayefanya naye kazi.

“Asije mtu huko akawadanganya kuwa eti Mwenyekiti ama kiongozi yeyote wa ngazi za juu katoa maelekezo achaguliwe mtu Fulani.”, ameeleza Dkt. Magufuli.

Akiendelea kufafanua Rais Magufuli  amewambia Wajumbe hao kuwa uchaguzi huo ni muhimu sana kwa maisha na ustawi wa maisha marefu ya CCM na umoja huo na kuwasisitiza kufanya maamuzi sahihi ya viongozi watakaopambana na kushinda vikwazo vilivyomo katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa nchini.

Amesema wanatakiwa kuwachagua viongozi wenye uwezo na msimamo wa kukemea hadharani vitendo vya rushwa na ufisadi ndani ya Umoja wa Wazazi, Serikali na Chama cha Mapinduzi kwa ujumla.

Ameeleza kwamba anathamini umuhimu wa jumuiya hiyo ambayo ndio nguzo na chimbuko la ukomavu wa kisiasa wa CCM kwani imeanzishwa toka mwaka 1955 na waasisi wa Chama hicho kwa lengo la kusimamia mwenendo wa maadili ya chama hicho.

Aidha ameahidi kuwa ataendelea kushikamana na jumuiya hiyo kwa lengo la kuhakikisha inakuwa na nguvu zaidi kupitia rasilimali zake za kiuchumi na zinawanufaisha watu wote.

Kupitia mkutano huo ametangaza neema kwamba atazipa haki sawa jumuiya zote za chama hicho hasa katika nafasi za uteuzi wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili waweze kuwa na uwiano sawa katika chombo cha kufanya maamuzi na kutunga sheria.

Mapema akizungumza Mwenyekiti wa Umoja huo kabla ya kujiuzulu kupisha uchaguzi huo, Abdalla Bulembo amesema licha ya umoja huo kukabiliwa na changamoto nyingi lakini amemaliza uongozi wake umoja huo ukiwa na akiba ya fedha shilingi bilioni 2.1 .

Pia, ameeleza kwamba katika upande wa sekta ya elimu umoja huo unamiliki shule 54 kikiweo  Chuo kimoja kinachotoa mafunzo ya kuwajengea ujuzi wa kujitegemea vijana ambacho kinatoa taaluma kwa ngazi ya cheti na stashahada.

Mwenyekiti huyo alisema katika ziara mbali mbali zilizofanya na Umoja huo Tanzania nzima wamefanikiwa kuvuna wanachama 800,795 ambao ndio mtaji wa kisiasa wa umoja huo, sambamba na kupunguza madeni kwa asilimia 65 waliyokuwa wakidawa na mashirika mbali mbali ya umma na binafsi.

Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo Bulembo anayemaliza muda wake wa kuongoza Umoja huo, amempongeza Dkt. Magufuli kwa juhudi zake za kuwaunganisha Wanzania na kuwa mzalendo wa kweli katika kupigania haki za wanyonge.

Mkutano huo umeudhuriwa na wawakilishi wa Vyama mbali mbali vya upinzani ambavyo ni marafiki wa Chama cha Mapinduzi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni