Jumatano, 30 Januari 2019

HOSPITALI YA WILAYA KASKAZINI 'A' KIVUNGE YAKABIDHIWA VIFAA TIBA.


 MWENYEKITI wa Kikundi cha Hamasa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Ndugu Shaaban Ali Othman (kushoto) akimkabidhi Daktari dhamana Tamim Hamad Said(kulia)  Friji mbili za kuhifadhi dawa za hospitali zilizotolewa na kikundi cha hamasa cha vijana wa  Afisi Kuu CCM Zanzibar.

 
MWENYEKITI wa Kikundi cha Hamasa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Ndugu Shaaban Ali Othman (wa pili kushoto) akizungumza mara baada ya kuwasili katika Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Daktari dhamana Tamim Hamad Said (wa kwanza kushoto) pamoja na Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Haji Machano Juma(wa kwanza kulia) wakiwa katika hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na kikundi cha hamasa.

 KATIBU wa Kikundi cha Hamasa  cha Afisi Kuu ya CCM Zanzibar ndugu Suleiman Mohamed Rashid (wa kwanza kushoto aliyesimama) akizungumza katika kikao cha hafla ya makabidhiano ya mafriji mawili yaliyotolewa na kikundi cha hamasa.

 KATIBU wa CCM Wilaya ya Kaskazini 'A' ndugu Haji Machano Juma akizungumza katika hafla hiyo.

 Daktari Dhamana wa Hospitali hiyo Tamim Hamad Said, akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano ya mafriji ya kuhifadhi  dawa.

 Katibu Msaidizi wa Taasisi hiyo Ndugu Khamis Salum Abdi , akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa na CCM.

 Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Pandu Salum Sungura .

 BAADHI ya vijana wa kikundi cha hamasa cha Afisi Kuu ya CCM Zanzibar wakisikiliza kwa makini nasaha za viongozi mbali mbali wa CCM, UVCCM na Hospitali ya Wilaya Kivunge katika hafla ya makabidhiano ya Vifaa Tiba iliyofanyika leo Tarehe 30/01/2019

 Picha ya pamoja  ya Wajumbe wa Kikundi cha Hamasa cha Afisi Kuu ya CCM Zanzibar pamoja na Uongozi wa Hospitali ya Wilaya Kivunge , Mkoa wa Kaskazini Unguja, mara baada ya hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba.
 
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
VIJANA mbali mbali nchini wameshauriwa kuendeleza utamaduni wa kujitolea katika kuisaidia jamii katika masuala mbali mbali ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kimaendeleo.

Rai hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kikundi cha Hamasa cha Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Ndugu Shaaban Ali Othman wakati akikabidhi Friji(Jokofu) mbili zilizotolewa na kikundi hicho na kukabidhi Uongozi wa Hospitali ya Kivunge ya Wilaya Kaskazini 'A' Unguja.

Amesema vifaa hivyo vimetolewa kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa vifaa tiba vya hospitali hiyo hasa dawa za matumizi ya binadamu zinazohitaji hali ya baridi muda wote.

Ameutaka uongozi wa Hospitali hiyo kuvitunza na kuvitumia katika matumizi yaliyokusudiwa ili vitoe huduma endelevu kwa wananchi mbali mbali wanaofika hopitalini hapo kwa ajili ya matibabu.

Pamoja na hayo amebainisha kuwa vifaa hivyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wa CCM ambao ni Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein wanaotekeleza kwa kasi  mipango ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi wote.

Ameeleza kwamba vijana nchini wana wajibu wa kutekeleza kwa vitendo masuala mbali mbali ya kijamii kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto katika mazingira wanayoishi.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Shaaban,amesema endapo vijana wa Zanzibar wataweka mbele dhana ya uzalendo,umoja, mshikamano na kuelekezana mambo mema ya kuisaidia jamii, itasaidia Zanzibar kuwa nchi bora zaidi duniani iliyopiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Awali Katibu wa Kikundi hicho cha Hamasa, Suleiman Mohamed Rashid amefafanua kuwa kikundi hicho kitaendelea kusaidia masuala mbali mbali ya kijamii katika maeneo mbali mbali yaliyopo katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Amesema Chama Cha Mapinduzi kipo mstari wa mbele kushughulikia changamoto  zinazoikabili jamii katika maeneo ya mijini na vijijini.

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Daktari Dhamana wa Hospitali hiyo Tamim Hamad Said, amesema uongoizi wa hospitali hiyo umefurahi kupokea vifaa hivyo kwani vilikuwa ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya taasisi hiyo.

Dr.Tamim ameahidi kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa hasa kuhifadhi dawa na vifaa mbalimbali vinavyotumika katika matibabu ili wananchi wapate huduma bora za Afya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Pandu Salum Sungura amesema vijana wa mkoa huo wapo imara katika kuunga mkono juhudi za vijana wenzao wa kikundi cha hamasa kutoka Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, kilichoonyesha mfano bora wa kutoa vifaa hivyo kwa hospitali ili viwasaidie wananchi wa Mkoa huo.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, Katibu Msaidizi wa Taasisi hiyo Ndugu Khamis Salum Abdi amesema Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kusimamia na kutekeleza Ilani yake ya Mwaka 2015/2020 kwa ufanisi mkubwa kwa lengo la kumaliza kero zinazoikabili jamii.

Amesema suala la kuwapelekea wananchi maendeleo halina itikadi za kisiasa hivyo kila mwananchi, kikundi pamoja na taasisi yoyote wana wajibu wa kutatua changamoto za wananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni