Jumamosi, 18 Agosti 2018

DK.BASHIRU AWAPIGA MSASA VIJANA 1560, DK. MABODI ASEMA CCM INATEKELEZA SERA KWA VITENDO .

 KATIBU Mkuu wa CCM Tanzania Dk.Bashiru Ally akizungumza na makundi mbali mbali ya Vijana katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani Unguja

 BAADHI ya vijana wa UVCCM kutoka makundi mbali mbali walioudhuria mkutano huo.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Tanzania Dk.Bashiru Ally amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa ya elimu ili wapate ujuzi na maarifa ya kulinda na kusimamia rasilimali za nchi  zisiporwe.

Rai hiyo ameitoa leo katika mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha visiwa humo wakati  akizungumza na vijana kutoka makundi mbali mbali ya Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa wa Mjini uliopo Amani Unguja.

Amesema elimu ndio njia pekee ya kuwajenga vijana wa CCM kuwa na fikra chanya za kulinda tunu za taifa lao zisihujumiwe bali ziendelezwe kwa lengo la kuvinufaisha vizazi vya sasa na vijanavyo.

Akizungumza na vijana zaidi ya 1560 kutoka katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, ameeleza wazi kuwa elimu hiyo itakuwa na manufaa zaidi endapo makundi hayo yatafuzwa siasa na itikadi zinazoeleza historia halisi ya nchi yao ili wapate ujasiri wa kulinda Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa vitendo.

Dk.Bashiru amesema vijana waliopikwa kiitikadi na kurithishwa siasa za ukombozi na ulinzi juu ya misingi ya kitaifa, wanakuwa madhubuti katika kuendeleza kwa kazi Nyanja mbali mbali za kijamii, kiuchumi kisiasa.

Katika kutilia mkazo malengo hayo Chama kinajenga Chuo Kikuu cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo  kibaha Mkoani Pwani, ambacho kitatoa viongozi walioiva na kubobea katika siasa zenye tija zinazolinda misingi ya kitaifa kwa maslahi ya jamii.

“ Vijana hamuwezi kulinda Mapinduzi ya Zanzibar wala azimio la Arusha bila kujielimisha juu ya historia ya taifa lenu ambalo ndio chimbuko ya vuguvugu la ukombozi wa nchi mbali mbali za bara la Afrika.”amesema Dk.Bashiru.

Akizungumzia kuimarika kwa misingi ya demokrasia nchini amesema viongozi wa CCM ndio walioasisi na kutoa baraka zote juu ya mfumo huo.

Pia amesema milango ya Tanzania ipo wazi kwa mataifa yanayotaka kuja kujifunza demokrasia hapa nchini kwani mfumo huo unazidi kuimarika kila kukicha.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa baadhi ya vikundi vinavyojiita vyama vya kisiasa na kutumiwa vibaya na mataifa ya kigeni visiporudi katika mstari vitakufa kifo cha mende.

Katika mkutano huo Katibu Mkuu huyo amezitaja sababu za CCM kuwa na mvuto kwa wananchi kwa kueleza kwamba kwa sasa imerudi kwa wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.

Sababu nyingine amesema ni kutokana na viongozi wakuu wa Serikali zinazotokana na CCM ambao ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ni wasafi kiungozi hawana kasoro za vitendo viovu vya rushwa na wizi wa mali za umma.

“ Hizo ndio sababu za wapinzani kujiunga na CCM kwani huko walipokuwa katika vyama vya upinzani kumejaa ubabe, rushwa na mifumo dume ya kukandamiza haki na fursa za vijana na wanawake”, ameendelea kueleza Dk.Bashiru.

Amewataka vijana kuendelea kuiunga mkono CCM kwa kuhakikisha mwaka 2020 inashinda kwa lengo la kusimamia umoja,amani, utulivu na maendeleo endelevu kwa wananchi wote.

 Akizungumzia usimamizi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa upande wa Zanzibar, amempongeza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Mabodi kwa kasi yake ya kuisimamia serikali kutekeleza dhana hiyo inayowaletea wananchi maendeleo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dk.Abdulla Juma  Mabodi amesema CCM kwa upande wa Zanzibar inaendelea na kazi ya kufanya siasa za ushindani wa sera kwa vitendo zinazotekelezeka na sio maneno matupu.
Dk.Mabodi amesema katika juhudi za kuimarisha taasisi hiyo kubwa ya kisiasa imeamua kuwa karibu zaidi na vijana wa rika tofauti kwa kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Mapema akizungumu Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita, amesema vijana hao wapo imara na watahakikisha wanatekeleza kwa vitendo Ibara ya 5 ya katika ya CCM ya mw aka 1977 toleo la mwaka 2017 kwa kuhakikisha CCM inashinda uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 pamoja na serikali kuu mwaka 2020.

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Mohamed Rajab Soud amempongeza Katibu Mkuu wa hotuba zake nzuri zenye na kuahaidi kuwa viongozi hao watayafanyia kazi kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM kwa la lengo la kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Mkutano huo umehitimisha ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dk.Bashiru Ally kwa upande wa Unguja,  ambapo kesho anatarajia kuendelea na ziara hiyo Kisiwani Pemba kwa kuzungumza na viongozi wa CCM na jumuiya zake pamoja na makundi mbali mbali ya vijana wa Mikoa miwili ya Kichama.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni