Jumapili, 6 Mei 2018

DK.SHEIN-ASEMA WANAOKWEPA KUTEKELEZA ILANI WASIPE FOMU ZA KUGOMBEA UONGOZI


 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akiwahutubia na mabalozi wa CCM Wilaya ya kaskazini ''A'' Unguja.

 MAKAMU Mwenyuekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein mara baada ya kuwasili katika Afisi ya CCM Mkoa wa kaskazini mahonda katika mwendelezo wa ziara zake za kuzungumza na mabalozi wa CCM Wilaya ya kaskazini ''A''.
 BAADHI ya mabalozi wa CCM Wilaya ya kaskazini'' A'' wakifuatilia kwa makini hotuba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdalla Juma Mabodi akizungumza na mabalozi wa CCM Wilaya ya kaskazini 'A' Unguja.

 MAKATIBU wa Idara Maalum ya NEC CCM Zanzibar wakijitambulisha kwa mabalozi wa CCM Wilaya ya Kaskazini Unguja.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita (kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa UWT  Taifa Thuwayba Kisasi (kulia) wakiwasalimia mabalozi wa Wilaya ya kaskazini ''A''.

 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akionyesha Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020.

 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akisisitiza umuhimu wa mabalozi kusoma Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, kutowapatia fomu za kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao  Wabunge, Wawakilishi na madiwani wanaoshindwa kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Pia Dk. Shein amesema suala la viongozi hao kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM sio jambo la hiari bali ni lazima kwa kiongozi yeyote aliyepewa ridhaa ya kuwatumikia wananchi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Agizo hilo amelitoa katika mwendelezo wa ziara zake wakati akizungumza na mabalozi wa CCM Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja, huko katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja-Mahonda.

Dk.Shein alisema kiongozi yeyote ndani ya CCM anayeshindwa kutekeleza kwa wakati ahadi alizotoa kwa wananchi asipewe nafasi nyingine ya kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Aliwambia mabalozi hao kwamba CCM haitowaonea huruma Wabunge, Wawakilishi na Madiwani waokwepa kutekeleza majukumu yao na badala yake kukiletea Chama mzigo mkubwa wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

"Wakumbusheni Wabunge, Wawakilishi na madiwani kutekeleza ahadi zao kwa wakati na wakikataa basi katika uchaguzi mkuu ujao msiwape fomu za kugombea tena.", alisisitiza Dk. Shein.

Agizo hilo Dk.Shein alilitoa kufuatia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Idd Ali Ame kusema kuwa  Kamati ya siasa ya Mkoa wake tayari imefanya ziara ya kuimarisha Chama katika majimbo tisa(9) ya mkoa huo na kupokea malalamiko ya baadhi ya viongozi hao wa majimbo kushindwa kutekeleza ahadi walizoahidi kwa wananchi.

Akizungumza katika Mkutano huo Dk.Shein alisema Chama Cha Mapinduzi kinawategemea na kuwaamini mabalozi katika kulinda, kutetea na kukiletea ushindi Chama kwa kila uchaguzi kwani wao ndio waliokuwa karibu zaidi na wananchi wa makundi yote.

Amewataka mabalozi hao kulinda maadili, miongozo na miiko ya Chama Cha Mapinduzi ili taasisi hiyo ya kisiasa iendelee kubaki katika misingi yake ya kiuongozi na ustawi wa demokrasia.

 Pamoja na hayo hayo Dk. Shein alisema hafurahishwi na kuripotiwa kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto, hivyo mamlaka husika zinatakiwa kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaofanya matukio hayo.

Aliwakumbusha mabalozi hao kuwa mstari wa mbele kutangaza mambo mema yanayotekelezwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili wananchi waliopo katika maeneo yao waweze kuyafahamu.

Dk.Shein alisema serikali inaendelea na jitihada za kutekeleza miradi ya kimaendeleo kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa barabara za kisasa ndani ya Mkoa huo za maeneo ya Mkwajuni-Kijini km 7.6.

Zingine ni barabara za Mkwajuni-Mbuyu maji km 22, Pale-Kiongele km 4.6 pamoja na Bububu-Kinyasini zote zikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Aidha Dk.Shein alisema serikali ina dhamira ya kujenga mji wa kisasa katika eneo la Mkokotoni ili kwenda sambamba na dhana ya kuifanya Zanzibar kuwa na miji ya kisasa.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi ameeleza kuwa viongozi wa chama na serikali wamekuwa wakishirikiana vizuri katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Dk.Mabodi amesifu juhudi za kuimarisha Chama Cha Mapinduzi zinazofanywa na uongozi mpya wa Mkoa huo kuwa zinajenga matumaini na uaminifu kwa Wana-CCM.

Akisoma risala ya mabalozi, Jafar Ali Haji alisema wanampongeza Dk.Shein kwa kuendelea kuongoza serikali kwa ufanisi mkubwa, sambamba na kusimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo.

"Tunakupongeza Dk.Shein kwa mambo mengi mazuri uliyoyafanya kwa maslahi ya wananchi wa Wilaya ya Kaskazini 'A' na maeneo mengi hasa kuanzisha mfuko ya pencheni ya wazee tunayopata shilingi 20,000 kwa kila mwezi.

Kupitia risala hiyo walieleza kuwa tayari maagizo ya Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, aliyotoa katika ziara zake za kiserikali mwaka jana yametekelezwa kwa kiwango kikubwa katika vijiji vya Mbuyu tende na Mlilile na kwa sasa wananchi wa  wanapata huduma za maji safi na salama, skuli na barabara.

Mabalozi hao walisema licha ya mafanikio hayo bado Wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kwa ngazi ya sekondari na msingi pamoja na upungufu wa wauguzi katikka vituo vya Afya ya Wilaya hiyo hasa kituo cha Kivunge. 

                                


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni